Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, wanazuoni wa Bahrain wamezindua kaulimbiu ya mwezi wa Muharram na siku za maombolezo ya Imam Abu Abdillah Al-Hussein (as) kwa mwaka 1448 Hijria Qamaria kwa anuani isemayo:
«لا معبود سواك»
“Hakuna anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Wewe.”
Wanazuoni katika taarifa yao walitangaza kwamba: Karbala katika kila zama huendelea kuwa hai kwa sura tofauti, na damu ya Imam Hussein (as) katika kila zama humwagwa na watu waovu zaidi miongoni mwa waovu.
Suala kuu ni suala la njia mbili: njia inayolingania kuabudiwa kwa twaghuti, na njia inayolingania kumuabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambayo kaulimbiu yake ya milele ni: “Hakuna anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Wewe.”
Taarifa hiyo iliongeza kuwa: “Njia ya Imam Hussein (as) ni njia ya risala za mbinguni ambazo zimeendelea katika historia yote hadi pale Mwenyezi Mungu atakaporithi ardhi na vilivyomo juu yake.
Njia hii ni njia ya imani, uchamungu, uongofu, marekebisho, nuru, uadilifu, jihadi, subira, kujitolea, kujitoa muhanga na maana zote za kheri, mema, ukamilifu na maisha ya juu ya kibinadamu; maisha ambayo hayawezi kupatikana isipokuwa chini ya kivuli cha kujikomboa kutokana na kuabudu matamanio ya nafsi, kumuabudu twaghuti na shetani, pamoja na kila sanamu linaloshusha thamani ya mwanadamu na kumuangusha katika daraja za chini kabisa kiasi kwamba anakuwa mpotovu zaidi kuliko wanyama.”
Wanazuoni wa Bahrain walieleza: “Muumini, kwa muda wote anapokuwa mja mtiifu wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, maana yake ni kwamba yuko katika njia ya ukamilifu na ameacha njia itakayo sababisha kuporomoka kwa moyo wake, akili yake, mwenendo wake na katika nyanja zote za maisha yake ya kimwili na kiroho, na ataendelea kumfuata Bwana wa Vijana wa Peponi (as) hadi pumzi yake ya mwisho duniani.”
Wanazuoni wa Bahrain walifanya upya ahadi yao kwa Imam Hussein (as), njia yake na mwenendo wake, na wakatangaza kaulimbiu ya milele ya tauhidi ya Kihussein:
«لا معبود سواك»
Hakuna anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Wewe.”
Kaulimbiu hiyo inalenga kuifanya itikadi ya tauhidi kuwa mhimili mkuu na wa msingi katika nyanja zote za harakati za marekebisho ya Umma wa Kiislamu, kuimarisha imani ya kukataa aina yoyote ya utumwa kwa asiye Mwenyezi Mungu, na kupuliza roho ya subira ya kimkakati na uimara katika kukabiliana na matatizo.
Walitoa wito kwa wanazuoni wote, makhatibu, Waislamu wote, taasisi, watu mashuhuri na wanaharakati wa Hussein kushirikiana katika kuitangaza kaulimbiu hii ya Kihussein na kuiendeleza katika nyanja za kielimu, kivitendo na kitamaduni, ili kuinua hali yetu kuelekea katika nafasi inayoridhiwa na Mola anayestahiki kuabudiwa.
Maoni yako